Shabiki wa klabu ya Sunderland wa umri wa miaka sita Bradley Lowery, ambaye tatizo lake la kiafya liligusa nyoyo za wengi amefariki dunia.
Bradley alikuwa anaugua ugonjwa ambao wa Kiingereza hufahamika kama neuroblastoma - aina nadra ya saratani - tangu alipokuwa na umri wa miezi 18. Bradley alifanywa kuwa shabiki -nembo ya klabu hiyo na akaunda urafiki wa karibu na mshambuliaji wa klabu hiyo Jermain Defoe.
Aidha, aliongoza wachezaji wa England kuingia uwanjani Wembley wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Lithuania. Kifo chake kimethibitishwa na wazazi wake kwenye mitandao ya kijamii.
"Kijana wetu mkakamavu ameenda kuwa na malaika leo. "Alikuwa shujaa wetu na alipigana sana lakini alihitajika kwingine. Hatuna maneno ya kueleza jinsi tulivyohuzunishwa na kifo chake." Mamayake Bradley Gemma Lowery alikuwa akilia amesema mvulana huyo alikuwa amedhoofika sana Bradley alipewa matibabu lakini saratani yake ikaibuka tena mwaka jana.
Wahisani walichangisha zaidi ya £700,000 kulipia matibabu yake New York mwaka 2016, lakini madaktari waligundua kwamba saratani yake ilikuwa imeenea sana na hangeweza kutibiwa. Wazazi wake Gemma na Carl, kutoka Blackhall Colliery, Durham, waliambia Desemba kwamba alikuwa amesalia na "miezi kadha tu ya kuishi".
Miezi minne baadaye, walifahamishwa kwamba jaribio la mwisho kabisa la kumtibu lilikuwa limefeli. Bradley aliipenda sana Sunderland AFC na alikaribishwa uwanjani Stadium of Light.
Bradley Lowery alipendwa na maelfu ya watu na alipokea kadi 250,000 za kumtakia heri wakati wa Krismasi, kutoka kwa watu mataifa ya mbali kama vile Australia na New Zealand.
TUTAKUMBUKA DAIMA BRADLEY.