Mkazi mmoja wa kijiji cha Kalunde kilichopo Kata ya Kipande wilayani Nkasi Vedasti Kazumba 51 amejiua kwa kujinyonga kwa kile kinachodaiwa kuwa alighadhabika baada ya Mkewe kumnyima kitoweo cha Samaki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa George Kyando alithibitisha tukio hilo na kusema lilitokea usiku wa mkesha wa mwaka mpya na kwamba Kazumba alifikia uamuzi huo mgumu kwa kujinyonga akitumia kamba ya Katani.
Alieleza hakuna mtu anayeshikiliwa na Polisi kuhusu tukio hilo na Uchunguzi wake unaendelea.
Habari kutoka kijijini humo kinaeleza kuwa chanzo cha Kazumba kujinyonga ni kukasirishwa na kitendo cha mkewe Antoniata Mwisua kumnyima kitoweo cha Samaki.
"Mke wa marehemu aitwae Antoniata alimwandalia mumewe huyo chakula cha Usiku kitoweo chake kikiwa ni Samaki mbichi Alimkomba samaki huyo kisha akamwomba amwongezee kitoweo kingine cha Samaki,lakini mkewe alimweleza kitoweo kimekwisha ndipo mumewe alipokasirika akidai kuwa
Mkewe amemnyima kwa makusudi kitoweo hicho ndipo alipochukua hatua ya kuzira kula" alieleza mmoja wa mashuhuda kwa masharti ya kutotajwa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kalunde John Kalasa alidai kuwa marehemu wakati wa Uhai wake alikuwa ni mtu mwenye kujawa na Ghadhabu ambapo Mara kadhaa alisikika akitishia kujinyonga.