Jeshi la polisi mkoani Pwani limezungumzia kifo cha askari wake PC Armand Furaha 33 aliyejipiga risasi kifuani bila kukusudia na kufariki dunia.Askari huyo alijipiga risasi hiyo usiku akiwa anaelekea kwenye lindo nyumbani kwa mkuu wa Wilaya ya Kibaha.Tukio hilo lilitokea saa 1 usiku eneo la Maili moja wakati askari huyo akiwa njiani
kuelekea kwenye kituo cha lindo alichopangiwa.
Kaimu kamanda wa polisi Pwani Blasius Chatanda amesema askari huyo alijipiga risasi kwa bahati mbaya kwa bunduki aina ya SMG akiwa amekaa kwenye kiti cha mbele katika gari alilokuwa anasafiria kwenda lindoni.Amesema uchunguzi wa awali umebaini "kuwa askari huyo alikuwa tayari ameweka risasi chemba kwenye bunduki hiyo aliyokuwa nayo na kwa bahati mbaya akiwa anashuka kwenye hilo gari ndipo risasi hiyo ikafyatuka na kumpiga kifuani eneo la kushoto na kufa wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Tumbi".
Kabla ya tukio hilo askari huyo aliwasili kazini jioni na kukuta amepangiwa kituo cha ulinzi cha Mkuu wa Wilaya hivyo kama ilivyo ada alichukua zana za kazi ikiwemo bunduki hiyo na kuanza safari ya kuelekea lindoni kwake huko kwa DC.
Lakini kwa bahati mbaya hakufika alikufa kwa kujipiga risasi bahati mbaya amesema Chatanda.
Akizungumzia suala la kujipiga risasi msemaji wa jeshi la Polisi,Advera Bulimba amesema kila tukio hutokana na mazingira tofauti.