Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olastiki jijini Arusha Hamisi Amani 17 kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Charles Mkumbo tukio hilo lilitokea Disemba 25 mwaka huu saa 2 usiku katika eneo la kwa Morombo.Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu kuwa ni Novatus Tadei 25 mkazi kwa Mrombo aliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani upande wa Kushoto.
Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye Kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiry Ally."Siku ya tukio marehemu pamoja na wafanyakazi wengine akiwemo mtuhumiwa baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya walipanda gari aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani.
"Wakiwa ndani ya Gari hilo mtuhumuwa Hamisi aligundua kuwa SODA aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.Kwa hiyo ulizuka Ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati Ugomvi huu ukiendelea mtuhumiwa alimkaba Marehemu na kuchukua KISU wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani"alisema Kamanda.
"Baada ya kumchoma kisu Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana kwani alifariki wakati anapelekwa Hospitali kwa ajili ya Matibabu"aliongeza Kamanda Mkumbo.
Aidha Kamanda Mkumbo alisema mwili wa Marehemu umehifadiwa katika Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru na Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya Uchunguzi kukamilika.